(ABNA24.com) Utafiti uliofanywa katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi vya homa ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaonyesha kuwa, kuna watu wengi ambao wanafia majumbani kwa Ebola kutokana na kukataa kwenda katika vituo vya afya.
Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, kwa akali watu 30 wameaga dunia kwa Ebola majumbani nchini humo katika kipindi cha wiki pekee za mwezi huu wa Julai.
Timu za wataalamu na madaktari sasa zimeanzisha msako wa nyumba hadi nyumba ili kuwagundua watu wanaogua maradhi ya Ebola ambao wameamua kukaa nyumbani badala ya kwenda katika vituo vya afya.
Rai wengi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo bado hawaamini kama kweli wanaofariki dunia nchini humo vifo vyao vinasababishwa na virusi vya homa ya Ebola.
Baadhi ya familia zina imani potofu na zinakataa kuwapeleka ndugu zao katika vituo vya afya zikiamini kwamba, wagonjwa wanaoaga dunia katika vituo hivyo vya afya, wanauawa na si kweli kwamba, wanakufa kwa Ebola.
Watalaamu wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema kuwa, bado kuna changamoto kubwa zinazozikabili juhudi za kieneo na kimataifa za kukabiliana na maradhi ya Ebola.
Wakati huo huo, serikali ya Saudi Arabia imetangaza kkuwa, haitatoa viza ya kusafiria kwa mahujaji watarajiwa kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kutokana na hofu ya Ebola. Waislamu 410 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walitarajiwa kwenda kufanya ibada ya Hija mwaka huu.
/129